SEHEMU YA TATU

 SIMULIZI: HATIA TAKATIFU


Mwandishi: Kedmund Mtembezi

Email kedmund742@gmail.com

WhatsApp+255 672 229 424


SEHEMU YA 3:


Siku chache zilipita tangu ile kazi ya kwanza. 

Maisha ya Kedmund yalianza kubadilika… taratibu, lakini kwa namna ya hatari.

Mfukoni kulikuwa na pesa. Sio nyingi sana, lakini za kutosha kubadilisha hali ya nyumbani. Mama yake alianza kupika vizuri zaidi, na hata tabasamu lake lilianza kurudi.

Lakini kwa Kedmund…

Amani ilizidi kupotea.

Kila usiku alipolala, akili yake ilirudia ile tukio ya polisi. Ile hofu haikuisha. Ilibaki ndani yake kama kivuli kinachomfuata.

Siku moja jioni, akiwa amekaa na Juma pale pale kwenye jiwe lao la kawaida, simu ya Juma iliita.

Alipokea, akasikiliza kwa sekunde chache, kisha akakata.

“Rashid anakuita,” alisema.

Kedmund alinyanyua macho polepole.

“Leo tena?”

Juma alitabasamu kwa maana nzito.

“Hii sio kazi ya mara moja bro… umeingia game sasa.”

Walipofika tena kwenye ile nyumba, hali ilikuwa tofauti.

Safari hii, kulikuwa na watu wengine ndani. Wanaume wawili wenye sura ngumu, na mwanamke mmoja aliyekaa kimya kona akicheza na simu yake.

Macho yao yote yalikuwa na kitu kimoja — ukali.

Rashid aliingia akiwa na simu mkononi, akawaangalia Kedmund na Juma kwa utulivu.

“Mlifanya kazi safi,” alisema.

Juma alitabasamu. Kedmund alibaki kimya.

Rashid alimsogelea Kedmund.

“Lakini wewe…” alisema, “bado unaogopa.”

Kedmund hakujibu.

“Usiogope pesa,” Rashid aliendelea. “Oga hofu.”

Kila mtu ndani ya chumba alicheka kidogo.

Kedmund alihisi kama anazidi kushinikizwa kuingia ndani zaidi ya kitu ambacho hakielewi kikamilifu.

Safari hii, hawakupewa begi.

Walipata kitu tofauti.

Bahasha.

Ndogo.

Nyepesi.

Lakini Rashid alisisitiza:

“Hii ni muhimu zaidi ya ile mzigo wa jana. Hii haipaswi kupotea. Ukipoteza… maisha yako yanaweza kupotea pia.”

Moyo wa Kedmund uliruka.

“Hii ina nini?” aliuliza.

Rashid alimsogelea karibu sana, macho kwa macho.

“Usiulize vitu visivyokuhusu.”

Kimya kilitanda.

Safari hii hawakupanda daladala.

Walichukua bodaboda.

Walikuwa wanapita mitaani kwa kasi, upepo ukipiga uso wa Kedmund, lakini akili yake ilikuwa mbali kabisa.

Alihisi kama anazama polepole kwenye maji marefu.

Walipofika sehemu ya makaburi yaliyotelekezwa kidogo pembeni ya mji, Kedmund alishangaa.

“Tunafanya nini huku?” aliuliza.

Juma hakujibu.

Walikutana na mtu mwingine — kijana mdogo, lakini macho yake yalikuwa makali kuliko hata ya Rashid.

Alipokea ile bahasha bila kusema neno.

Lakini kabla hajaondoka, alimwangalia Kedmund kwa sekunde kadhaa.

Halafu akasema:

“Karibu kwenye mchezo wa kweli.”

Maneno hayo yalimfanya Kedmund atetemeke.

Wakiwa njiani kurudi, Kedmund hakuvumilia tena.

“Juma… hii ni kazi gani hasa?” aliuliza kwa hasira kidogo.

Juma alikaa kimya kwa muda, kisha akasema:

“Ni biashara bro… biashara ya watu wakubwa.”

“Biashara gani? Dawa za kulevya? Uhalifu?” Kedmund aliuliza moja kwa moja.

Juma alimtazama.

“Unataka kujua sana au unataka pesa?”

Swali hilo lilimchoma.

Kedmund alikaa kimya.

Ndani ya moyo wake, alijua jibu.

Lakini hakupenda ukweli huo.

Usiku huo, alipofika nyumbani, alimkuta dada yake akitabasamu.

“Kedmund! Leo nimepata nafasi ya kurudi shule!” alisema kwa furaha.

Kedmund alishangaa.

“Vipi?”

Mama yake alitoka jikoni.

“Hizi pesa ulizotuletea zimeanza kusaidia mwanangu… Mungu akubariki.”

Maneno hayo yalimchoma moyo.

Kwa sababu alijua…

Pesa hizo zina harufu ya hatari.

Lakini pia…

Zinaanza kubadilisha maisha yao.

Siku zilivyopita, Kedmund alianza kuzoea.

Hofu ilipungua kidogo.

Confidence ikaongezeka.

Pesa zikawa nyingi zaidi.

Lakini pia…

Alianza kuona vitu ambavyo hakutakiwa kuona.

Usiku mmoja, alipokuwa anarudi peke yake baada ya kazi, aliona gari likisimama ghafla karibu yake.

Mlango ukafunguliwa.

Wanaume wawili wakashuka.

“Mzee anataka kukuona sasa hivi,” mmoja alisema.

Hakukuwa na chaguo.

Aliingia kwenye gari.

Moyo wake ukianza kupiga tena kwa kasi ile ile ya mwanzo.

Safari hii, alihisi wazi kabisa:

👉 Anaingia ndani zaidi ya kitu kisicho na njia ya kutoka.

Na safari hii…

Hakuwa na uhakika kama ataweza kutoka salama.


 Mwisho wa Sehemu ya 3


#Like_comment Tuendelee sehemu ya 4.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

SEHEMU YA KWANZA

SEHEMU YA PILI

SEHEMU YA TANO